Asslaamu alaykum warahmatu llahi wabarakaatuh;
Shukurani zote anastahiki Allah, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume Muhammad.
Siku
zote inatakiwa muislam asiwe mwenye kuzembea katika mambo mbali mbali
yenye manufaa, khususani misimu ya utiifu kama vile Ramadhani. Bali
inatakiwa awe wa mwanzo katika twa’a hizo na awe ni mwenye kushindana na
kuhakikisha ya kwamba hakuna anaye mpita.
قال الله تعالي:( وَفِي ذَلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ)
المطففين:26
Anasema Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
(Na katika hayo {mambo ya kheri} washindanie wenye kushindana).
Suurat Al Mutwafifiin: 26
Imepita
miezi, mawiki na masiku na hivi sasa umekaribia Mwezi wa Qur‘an, mwezi
wa Baraka, mwezi wa ibada za usiku, mwezi wa kukubaliwa dua za waumini.
Ewe Allah tufikishe Ramadhani!
Maswahaba
walilelewa na madrasa ya Mtume wakihisi hisia hizi za kuwa na shauku
ya kuufikia mwezi wa fadhila, wakiishi na dua hii "Ewe Allah tufikishe
Ramadhaan!"
Wakawa wakimuomba Allah awafikishe Ramadhani kabla ya miezi sita, na miezi sita mingine wakimuomba Allah akubali ibada zao.
Bila
shaka hisia hizi na hali hii haikujengeka kwa Maswahaba isipokuwa kwa
kujua fadhila za mwezi huu, na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Je ili
tuweze kuupatia haki mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tunatakiwa
tufanyaje?
MAANDALIZI YA MWEZI WA RAMADHANI:
Bila
shaka shughuli yoyote ile huwezi kuifanya vizuri isipokuwa mpaka uwe na
utaalam nayo na umeifanyia mazoezi. Tuchukulie mfano michezo, iwapo
kama timu itakuwa na mechi basi hutenga muda maalumu kwa ajili ya
mazoezi ili kujiweka fiti na mechi hiyo. Licha ya kwamba wana utaalamu
na mpira lakini yawapasa wafanye mazoezi ili waweze zimudu pirika za
uwanjani.
Vile
vile ibaada mbali mbali ikiwemo funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani
inahitaji ujuzi na maandalizi, ili tuweze kuzikusanya fadhila mbali
mbali zilizomo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ikiwemo kufutiwa
madhambi, kukubaliwa ibaada hiyo ya funga na mengineyo.
Maandalizi hayo ni:
1. Kumuomba Allah Atufikishe Ramadhani
Kukithirisha kumuomba Allah atufikishe katika mwezi wa ramadhani "Ewe Allah tufikishe Ramadhani":
Masiku
haya ambayo tumeukaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani inatubidi tuzidishe
sana kumuomba Allah atufikishe ramadhani.Kwani kufikishwa ramadhaani ni
moja ya neema za Allah.Watu wengi watamani kufikkishwa mwezi mtukufu wa
ramadhani lakini si kila mmoja anaye tamani ataufikia.Kuna baadhi ya
watu tulikuwa nao ramadhani iliyo pita lakini mpaka hivi sasa hatupo nao
tena.Kwa hiyo sie tulio ruzukiwa uhai mpaka hivi sasa yatubidi
tujitahidi kumuomba Allah atufikishe mwezi huu mtukufu wa ramadhani
mwezi wa fadhila"Ewe Allah tufikishe ramadhani".
2. Kukithirisha kufunga katika mwezi wa shaabani:
Ni sunna kukithirisha swaumu katika mwezi wa shaabani kwa ajili ya kuiweka sawa nafsi kwa ajili ya kuupokea mwezi wa ramadhani.
Na hii ndio ilikuwa hali ya mtume,kama anavyo simulia Ummu al mu-uminiina Aisha radhi za Allah ziwe juu yake
(مَا
رَأَيْتُ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَ سَلَّمَ
اسْتَكْمَلَ صِيَامَ شَهْرٍ قَطُّ إِلَّا رَمَضَانَ وَ مَا رَأَيْتَهُ فِيْ
شَهْرٍ أَكْثَرَ صِيَاما مِنْهُ فِيْ شَعْبَانَ)
رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
(Sikumuona
Mtume anakamilisha swaumu mwezi mzima isipokuwa Ramadhani. Na sikumuona
anakithirisha funga katika miezi kama alivyo kuwa akikithirisha kufunga
katika mwezi wa Sha'baani)
Hadithi imepokelewa na Bukhari.
Kwa
hiyo yapendezwa kuanza kufunga tokea mwanzo mwa mwezi wa Sha’aban, vile
vile siku tatu katika mwezi; yaani ayyaamul baidh (Siku za tarehe13,14
na15 za kalenda ya Hijri) Vile vile siku ya Jumatatu na Alkhamis.
NB: Haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani
عَنْ
أَبِىْ هُرَيْرَةَ رَضِىَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ:قَالَ رَسُوْلُ الْلَّهِ
صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:(لَا تُقَدِّمُوا رَمَضَانَ بِصَوْمِ
يَوْمٍ وَلَا يَوْمَيْنِ إِلَّا رَجُلٌ كَانَ يَصُوْمُ صَوْما
فَلْيَصُمْهُ)
رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Imesimuliwa
kutoka kwa Abu Huraira radhi za Allah ziwe juu yake kasema: Kasema
Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake (Msitangulize Ramadhani kwa
kufunga siku au siku mbili, isipokuwa kwa yule aliye kuwa akifunga
kabla yake basi afunge)
Hadithi imepokelewa na Muslim.
Yaani
haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani isipokuwa kwa
yule aliyekuwa akifunga kabla. Mfano kwa yule aliyekuwa akifunga siku ya
Jumatatu na Alkhamisi. Basi ikidondokea moja ya hizo siku kabla ya
Ramadhani kwa siku moja au mbili hakuna tatizo kwa mtu huyu kufunga. Au
kwa yule mtu aliye panga kufunga mwezi wa shaabani karibia wote kama
alivyo kuwa akifanya mtume basi hakuna tatizo. Au kwa mtu aliyekuwa
kajizoesha kufunga siku na kufuturu siku basi hakuna tatizo kwake
kufunga pia.
Vile
vile haitakiwi kufunga siku ya shaka. Na siku ya shaka ni siku ya
thelathini ya mwezi wa shaabani ikiwa usiku wake ulikuwa ni wenye
mawingu mengi kiasi kwamba ikawa hawezekani kujua kama kuna mwezi au
hapana.Imeitwa siku ya shaka kwa sababu katika hali hiyo ya mawingu
tunakuwa na shaka je mwezi umeonekana au hauja onekana?
Wanazuoni
wametofautiana kuhusiana na katazo la kufunga siku hii ya shaka. Je ni
katazo linalo fidisha uharamu wa kufunga siku hii au ni katazo linalo
fidisha karaha (yaani yachukiwa)kwa hiyo ni bora zaidi mtu asifunge?
Rai
yenye nguvu juu ya suala hili ni kwamba katazo hili linafidisha uharamu
kufunga siku hii kama inavyo onekana wazi katika hadithi za Mtume
(rehma na amani juu yake)
3. Kuishi na Qur ani:
Yatakiwa
kujitahidi katika kusoma Qur ani angalau juzu moja kwa siku, ili mpaka
unaisha mwezi wa shaabani unakua ushakhitimisha Qur ani japo mara moja.
Vile vile yatakiwa kutenga muda maalumu kwa ajili ya kusoma na
kuzingatia aya mbali mbali katika Qur ani na wala si kutosheka kwa
kuisoma haraka haraka tu.
4. Qiyamu llayli:
Yatakiwa
kujitahidi kuswali ibaada za usiku tahajudi na witri; japo raakaa
mbili tahajudi na rakaa moja witri. Swali rakaa mbili kwa mazingatio.
Kumbuka swala ni mawasiliano kati ya mja na Mola wake. Wakati wa kuswali
hisi ya kwamba unazungumza na Allah na anakuona na kukusikia. Soma
suurat al Faatiha na sura baada yake kwa mazingatio na utulivu wa hali
ya juu, kwa kufanya hivyo utahisi radha ya ibada isiyo sifika na kuhisi
furaha ya maisha ya kweli. Kwani furaha ya maisha ya kweli inapatikana
katika kumtii Allah sub-hanahu wata’ala na kukithirisha ibaada mbali
mbali ikiwemo kuswali na ibaada za usiku. Na yule atakaye hisi ya kwamba
kumtii Allah na kutekeleza ibaada mbali mbali ni kujibana na kuto
yafaidi maisha basi dhana yake hiyo itakuwa ni potofu.
5. Kujifunza hukumu zinazo husiana na Ramadhani:
Inatakiwa
muislamu amuambudu Allah ‘azza wa jall kwa elimu au ujuzi, kwani kujua
hukumu za faradhi mbali mbali ambazo Allah ta’ala kazifaradhisha kwa
wanaadamu ni lazima kwa kila muislamu. Na katika faradhi hizo ni faradhi
ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa hiyo yatakiwa kujua hukumu
na mas’ala mbali mbali yanayo husiana na funga ya mwezi mtukufu wa
Ramadhani ili funga zetu ziwe sahihi na ziweze kubaliwa. Kwa hiyo
yatupasa kusoma vitabu mbali mbali vinavyo husiana na funga ya Ramadhani
na kuwauliza wenye elimu katika yale mambo tunayo tatizwa nayo.
Anasema mwenyezi Mungu mtukufu ndani ya Qur ani
فَاسْأَلوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لا تَعْلَمُونَ))
الأنبياء :7
(Basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.)
Al anbiyaa:7
6. Kuizoesha nafsi kwa kupunguza baadhi ya vyakula:
Inatakiwa
ujizoeshe kuacha baadhi ya vyakula licha ya kwamba wavipenda ili nafsi
yako itakapo fika Ramadhani iwe ishazoea hali ya kuacha baadhi ya mambo,
hali itakayo pelekea kufunga Ramadhani kiurahisi. Yatakiwa ujitahidi
kuipa dunia mgongo (Azzuhdi) kiasi kwamba mwezi wa shaabani kwako uwe
una tofauti kiasi na miezi mingine katika vyakula, vinywaji mavazi na
mengineyo. Mfano mzuri katika hili ni wale ambao huumwa na vichwa kwa
sababu ya kukosa chai asubuhi, basi inafaa kuanza kujizowesha kukosa
kunywa chai hata kabla ya mfungo wa Ramadhani ili ikifika Ramadhani
jambo hili lisikupe taabu.
7. Mazoezi ya ulimi:
Yatakiwa
ujizoeshe kusema ukweli na kuachana na uongo, usengenyaji na
ufitinishaji. Kwani mambo haya hayatakiwi yafanywe na muislamu yoyote na
kwa mfungaji basi makatazo yake ni ya hali ya juu. Haitakiwi mfungaji
awe ni mwenye kudanganya kusengenya na kufitinisha watu.
قَالَ الرَسُوْلُ
الله صَلَّى الله عَلَيْهِ وََسَلَّم: "مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّوْرِ
وَالعََمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِله حَاجَةٌ فِيْ أَنْ يَدَعَ طعَامَهُ
وَشَرَابَهُ" (رواه البخاري والترمذي وأبو داود وابن ماجه وأحمد)
Imetokana
na Abu Hurairah (Radhi za Allaah ziwe juu yake), Amesema Mtume rehma za
Allaah na amani zimshukie): “Yoyote ambaye hatoacha kauli za uwongo
(chafu) pamoja na matendo, basi Allaah hana yaja ya mtu huyu kuacha kula
na kunywa. (Imepokelewa na Bukhari, MuslimAbu Dawud, Ibn Majah na
Ahmad)
Hadithi hii itatuthibitishia kwamba ulimi mchafu ni tosha kuwa sababu ya kutokubali kwa funga ya mfungaji.
8. Kuihesabu nafsi:
Ni
bora kila mwisho wa siku ukakaa na kuihesabu nafsi yako umefanya
madhambi mangapi na kumtubia Allah na kuahidi ya kwamba huto rudia tena,
na kukumbuka adhabu ya moto, je mwili wako upo tayari kuishi motoni?
Bila shaka hii pia itakusaidia katika kutekeleza funga ya mwezi mtukufu
wa Ramadhani kwa ukamilifu. Kwani funga ya Ramadhani si kujizuia na
vyakula vinywaji na yale yenye kufuturusha, bali ni funga ya mauvo pia.
Lengo la funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kuwafanya watu wawe
wachamungu. Na uchamungu ni kufuata maamrisho ya Allah na kuachana na
makatazo yake.
Bila
shaka maandalizi haya iwapo kama tutayatekeleza kiukamilifu, basi ya
yanatosha kuwa sababu kuufunga mwezi wa Ramadhani kiukamilifu,
kiurahisi na kuhisi thamani ya Ramadhani na kutamani laiti mwaka wote
ungekuwa ni Ramadhani.
Ewe Allah tufikishe Ramadhani na ukubali ibada zetu, hakika Wewe ni Msikivu, Mjuzi wa yote na juu ya kila jambo ni Muweza.
No comments:
Post a Comment