MSATEKU

MSATEKU

Wednesday, 11 January 2017

VIPI MWANAFUNZI WA KIISLAMU ANATAKIWA AWE KATIKA SAFARI YA KUTAFUTA ELIMU

Kila msomi azingatie Ilani ya Elimu ya ‘Jabal Hirah’
Lengo lisiwe stashahada, astashahada, shahada ya msingi, Uzamivu na Uzamili tu pekee.
Je, Msomi wa Viwango vya juu ni aibu kuitwa Ustaadh?



Safari ya kila mwanafunzi wa Kiislamu kutoka nyumbani kwake kwenda shule/Chuo lazima iwe sawa na ile safari ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, kutoka nyumbani kwake kwenda pangoni, Jabal Hirah.

Kama ambavyo Mtume aliambiwa “Soma” kwa Jina la Mola wako basi kila mwanafunzi wa Kiislamu anatakiwa asome hivyo. Mwenyezi Mungu alimpa changamoto Mtume Wake kwa sura ya mwongozo.

Kwamba kila atakachokisoma akisome kwa ajili ya Mola wake. “Soma kwa Jina la Mola wako aliyeumba.” Kipande hiki cha aya za Mwanzo za Qur’an kinabeba maana kamili ya kusoma.

Aya hiyo ina maana kuwa chochote utakachokutana nacho katika kutafuta elimu kimeumbwa na Mwenyezi Mungu. Hii maana yake, kimsingi, ni kwamba vile vinavyosomwa ni matokeo ya kazi ya Mwenyezi Mungu.

Kwa ajili ya kutoa changamoto, Mwenyezi Mungu kaanza na baiolojia ya mwanadamu mwenyewe anayetakiwa kusoma, “Amemuumba mwanadamu kwa pande la damu.”

Mwenyezi Mungu hakutaka kuanza kwa kumpeleka mbali mja wake anayetafuta elimu bali kaanza na umbile lake mwenyewe. Aya hii inawasuta wale waliofanya jitihada za kutenganisha elimu inayoitwa ya dunia na ile ya dini.

Jitihada hizo mbaya zilikuwa na hila ya kumtenga Mungu na ile inayoitwa ‘elimu dunia’. Kwamba watu wavisome vilivyoumbwa bila kumjua aliyeviumba. Ulimwengu umezugwa na kuzugika kwamba Mungu atafutwe zaidi katika imani ya kiroho, na si katika maumbile aliyoyaumba.

Si ukweli wa kuficha kuwa ulimwengu umeachwa kwenye upofu wa kutomuona Mungu kwa hila iliyofanywa na Wapinzani wa Mungu. Mungu amebaki kama “dhana tu ya kiroho” ambapo kumwamini au kutomwamini kama yupo ni hiyari ya nafsi na si hitajio la kiakili.

Profesa wa Baiolojia hamuoni Mungu katika fani aliyosomea bali anamtafuta rohoni zaidi kwa mawaidha ya Msikitini ya Sheikh ambaye upeo wake juu ya maumbile si mkubwa kama ule wa Profesa.

Mwenyezi Mungu aliwahi mapema kutaka waja Wake wasome kwa Jina Lake, na kisha akaweka wazi mapema kuwa Yeye ndiye aliyeumba. Ilani hiyo ya Elimu iliukusanya mfumo mzima wa elimu ndani ya tauhiid.

Mosi, kulisoma pande la damu sio kusoma Fiqh wala thanawi bali ni kusoma sayansi ya Baiolojia ambayo, kwa hila za wapinzani wa Mwenyezi Mungu, imeitwa ‘elimu dunia’ ili eti msomaji wa sayansi hiyo asilihusishe somo hilo na dini.

Asome tu na kubobea, akikusanya vyeti vya kitaaluma, stashahada, astashahada, shahada ya msingi, shahada ya uzamili na uzamivu pamoja na kupewa heshima lukuki za kitaaluma.

Kazi nzuri yenye mshahara mzuri ndiyo lengo la msomi huyu. Gari nzuri ya kutembelea, nyumba nzuri ya kuishi, maisha mazuri ya kula na kunywa ndiyo yanayoonesha umuhimu wa jitihada alizozifanya za kutafuta elimu.

Kama hicho ndicho kilele cha jitihada za kutafuta elimu basi akili ya binadamu itakuwa imeishia pale ilipoishia ya mnyama napo ni pale pa kutafuta kula na kunywa.

Ilani ya Elimu iliyotolewa Jabal Hira inatupa mtazamo tofauti kabisa na huo. Mwanafunzi au Msomi wa Kiislamu lazima aizingatie Ilani hii. Kwa kuizingatia Ilani hii, kila somo linaingia na kufungiwa ndani ya dhana ya Tauhiid.

Wakati Qur’an ikitoa changamoto ya matumizi ya akili, na ikitoa dondoo za kisayansi katika aya mbalimbali ili kumkumbusha mwanadamu, msomi anapaswa kuielekeza akili yake katika fani yake, na kuisoma Qur’an kama Ilani ya Elimu yake.

Nguvu ya Tauhiid itakayojengeka kwa kuunganisha Aya za Qur’an na fani mbalimali za elimu itakuwa kubwa mno. Mwenyezi Mungu ataonekana kwenye Baiolojia, Kemia, Fizikia, Jiografia, Jiolojia, Hisabati na kadhalika.

Imani itakayojengeka hapa itakuwa ni ya yakini, sio ya mashaka-mashaka. Ibada itakayofanyika kwa msingi wa elimu hii itakuwa ni ibada ya hakika, sio ya mazoea na ya mkumbo.

Mwanafunzi atakayesoma kwa mtazamo huu hatahitaji kiboko cha kumswaga aende Msikitini, na moyo hautamruhusu kukwepa Swala. Mwanafunzi atakayesoma kwa mtazamo huu hatakuwa mtumishi wa tumbo lake, bali atakuwa Mtumishi wa Mola wake.

Akili ya msomi wa sampuli hii haitaishia kuijua falsafa ya fani yake bali itasumbuliwa na ishara za Muumba. Dhikiri au kumkumbuka Mwenyezi Mungu ambako huonekana kama ni utamaduni wa kiroho ndani ya Majumba ya Ibada nyakati za swala itachukua sehemu kubwa kichwani na moyoni mwa msomi huyu.

Kila wakati atatawaliwa na wingi wa utukuzo na shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kazi aliyoifanya, kuanzia akili inayomwezesha msomi kusoma kuja neema nyingine. Umbile lake mwenyewe kila siku na kila wakati litakuwa ishara mpya ya kumuona Muumba wake.

Anapovaa shati na kujitazama kwenye kioo, hatoishia kuona kuwa kapendeza bali ataona sanaa ya Mwenyezi Mungu katika umbo lake na mara moja ataisifu na kuitukuza Kazi ya Mola wake.

Msomi huyu hawezi kupitisha sekunde au dakika bila kulitafakari umbile lake, na umbile la Mbingu na Ardhi. Akijitazama mwenyewe au akiwatazama wanadamu wenziwe mara moja humuona Muumba wake.

Anapoyatazama macho yake mwenyewe au ya mwenziwe anayetazamana naye hutanabahi, ni Nani aliyeweka macho haya mawili yanayofanya kazi muhimu kwa ushirikiano wa ajabu na ubongo!

Kama anasomea sayansi ya macho basi ndio kabisa atatosheka na jicho tu kumuona Mola wake hata kabla ya kutazama neema nyingine. Macho anayosomea yatakuwa msingi wa tauhiid, na yatakuwa ishara ya kila siku ya kumuona Mola wake.

Kama anasomea kinywa basi atatosheka na mfumo wa kinywa kwa jinsi ulivyopangiliwa meno yenye kazi ya kukata na kutafuna, na atastaajabu, ni Nani huyu aliyekipangilia kinywa namna hii!

Kinywa anachokisomea na kubobea kwacho kitakuwa msingi wa tauhiid na ishara ya kila siku ya kumuona Mola wake. Kama anasomea fuvu la kichwa, basi atajiuliza wakati wote, ni Nani huyu aliyeweka fuvu gumu ili kuukinga ubongo ambao unahitaji kweli kukingwa?

Kwa nini ubongo umekuwa ndani, fuvu limekuwa nje, hebu ona madhara yanayotokea pale ubongo unapoathirika? Ni Nani huyu aliyeuwekea kinga muhimu ubongo? Laiti fuvu la kichwa lingekuwa laini na la kubonyea-bonyea, ubongo usingelikuwa salama hata kidogo.

Hivyo, kwa kuvuta tafakuri hii pale anaposomea fani yake, msomi wa mrengo huu, hubakiwa na jawabu la hakika kichwani mwake kuwa yeye na kile anachosomea ni matokeo ya kazi aliyofanya Mwenyezi Mungu.

Hivyo, fani yake ya fuvu la kichwa inakuwa msingi wa tauhiid. Moja kwa moja anamuona Mwenyezi Mungu katika elimu yake, na siyo kumtafuta kwenye mawaidha ya Sheikh.

Anayesomea jiografia husomea mzunguuko wa sayari, na huona umakini usio wa kawaida ambao tangu ulimwengu ulipoanza miaka dahari, sayari zimekuwa zikizunguuka kwa kasi bila ajali yoyote!

Kupatikana kwa usiku na mchana na mabadilikon ya majira ni matokeo ya mzunguuko huo. Msomi wa fani hii atakayezingatia Ilani ya Elimu ya Jabal Hirah muda wote atasumbuliwa na swali kichwani, ni Nani huyu aliyeumba mfumo wa sayari na kuuzunguusha kwa usalama ili kuleta mabadiliko ya nyakati, usiku na mchana na misimu ya masika, kiangazi, kipupwe na kadhalika?

Ni Nani aliyeumba Bahari yenye manufaa kwa wanadamu, na kitoweo cha samaki kinachokamilisha lishe yake? Ni Nani aliyeweka ekolojia ya mvuke wa maji unaoevukia angani kwa upepo wa miti kwa ajili ya kutengeneza barafu ambayo hatimaye huyeyuka na kuleta mvua ambayo ni muhimu kwa maisha ya viumbe vyote vya ardhini?

Bila maji, maisha yasingelikuwepo? Ni Nani huyu aliyeweka ekolojia hii muhimu? Msomi hapa atamuona Mungu kabla ya kwenda Msikitini. Yeye ndiye atakayemthibitisha Mungu kuliko Sheikh anayeamini kiroho zaidi.

Kumbukumbu ya Mungu itakuwa ya kudumu akilini mwake, na haitakuwa ile ya wakati wa swala pekee. Msomi wa Jiolojia naye ataitazama milima na kuona jinsi inavyoisaidia dunia isiyumbishewe na kasi ya mzunguuko wa dunia.

Bila milima, amani isingelikuwepo. Maisha yangelikuwa ya kutetemeshwa na kubidukabiduka wakati wote. Lakini vigingi vilivyowekwa kwa sura ya milima vinafanya kazi muhimu ya kuibakisha ardhi katika utulivu unaofanya watu waone kama vile hakuna mzunguuko wowote.

Mtu wa kawaida hupata tabu kuelewa pale anapoambiwa dunia inabimbilika kwa sababu mbona hatubimbiliki. Hii ni hisani kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo msomi wa jiolojia anapaswa kuiona na kuwafafanulia watu wasiojua ili kwa pamoja tuungane kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Jiografia ni somo la Kiislamu, na si somo la “kizungu”. Kuyasoma maumbile ya Mwenyezi Mungu kunamwakisi Muumba, hakumwakisi Mzungu. Ukisoma jiografia unamuona Mungu, sio Mzungu.

Mifano hiyo itoshe kuonesha athari za Ilani ya Elimu ya Jabar Hirah. Ilani hiyo haimfanyi msomi Muislamu aache kusoma kwa ajili ya Mola wake na badala yake ajiwekee lengo bandia la kusomea stashahada, astatashahada, shahada ya msingi, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu, na baadae kupata kazi nzuri basi!

Badala yake, Ilani hii ndiyo itakayotupatia Makhalifa wa kweli wa kusimamisha Ufalme wa Mwenyezi Mungu. Mapinduzi ya kiitikadi yatakuja yenyewe yakiwa ni matokeo ya athari za ilani hii ya Elimu.

Ilani hii ya elimu ndiyo itakayotupatia wasomi halisi wa Kiislamu katika kila fani. Mjumuiko wa fani hizi ndio unaojenga jamii ya wasomi wanaoweza kuendesha mambo ya dunia kwa kuzingatia maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Wimbo wa kusimamisha Uislamu, mwito wa Jihadi vyote haviwezi kupata matunda bila kutekeleza Ilani hiyo ya Elimu ya Jabal Hirah. Tunaweza kirahisi kuimba wimbo wa kusimamisha dola ya Kiislamu, na tunaweza kirahisi kuitisha jihadi lakini mwisho wa siku, wimbo hautachezeka, wala mwito hautatimia kama hatutapata Jamii ya watu waliosoma kwa Ilani hiyo.

Tunaposema Uislamu ni itikadi ya kimapinduzi basi maana yake ni kwamba kila eneo la maisha linahitaji wasomi wa mrengo wa Kiislamu. Huwezi kujenga Uchumi wa Kiislamu bila kusomesha wachumi kwa Ilani ya Jabal Hirah.

Tunapozungumzia kusimamisha Uislamu, na tunapozungumzia Jihadi, dira letu lazima liangaze mbali sana kwamba hatimaye tutakuwa watu wa aina gani wa kuendesha serikali, na tuna watu wa aina gani wa kupigana jihadi.

Kwa Uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa Malaika kutoka Mbinguni, Mtume angeliweza kusimamisha Uislamu siku ileile ya kwanza aliyopewa Wahyi Jabal Hirah.

Au angeliweza kupigana Jihad Maka badala ya kuhamia Madina. Lakini bado kulikuwa na kazi ya kuijenga jamii, kuwajenga watu wa kupigana Jihadi, kuwajenga watu wa kusimamisha Uislamu, na kuwajenga watu wa kutawala na kutumikia Dola ya Kiislamu.

Kwa nini Mtume aliyekuwa na Nguvu za Mwenyezi Mungu nyuma yake na msaada wa Malaika alihitaji miaka mingi kusimamisha Dola ya Kiislamu? Jihadi ni faradhi lakini ni matokeo ya jitihada za awali za kujenga jamii ya Kiislamu.

Kubwa kabisa katika jitihada hizo ni kusomesha watu elimu zote kwa kuzingatia Ilani ya Jabal Hirah. Tunahitaji diploma, digrii kwa kuzingatia ilani hiyo. Hapo ndipo dhana ya mapinduzi ya Kiislamu itakapotimia.

Kwa ujumla, Ilani hiyo ya Elimu ndiyo ya kuwakomboa Waislamu kifikra na kiitikadi. Itawatoa katika dhana potofu kuwa ‘ukisoma sana’ Chuo Kikuu hustahili kuitwa Sheikh au Ustaadh!

Itawajengea hali ya kujiamini kuwa uanataaluma hautenganishwi na usheikh wala uustaadh. Bali uanataaluma sahihi ni mchanganyiko wa yote hayo. Yeye huyo huyo awe Daktari, yeye huyo awe Profesa, yeye huyo huyo awe Sheikh na Ustaadh kwa maana ni msomi yuleyule anayesoma kwa Jina la Mola wake.

No comments:

Post a Comment