MSATEKU

MSATEKU

Thursday, 18 May 2017

MAHAFALI YA JUMUIYA YA WANAFUNZI NA VIJANA WA KIISLAMU TANZANIA (TAMSYA) VYUO VIKUU VYA MKOA WA MBEYA, 2017.


ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH.

SHUKRANI ZA DHATI NI ZAKE YEYE ALLAH (SW) MOLA WA VIUMBE WOTE, NA REHMA NA AMANI ZIMFIKIE MTUME WETU MUHAMMAD (SAW).
TAREHE 14/05/2017 ILIKUWA NI SIKU ADHWIMU, SIKU TAMU, SIKU YA MASHAMSHAM AMBAYO WANAJUMUIYA YA WANAFUNZI WA KIISLAMU WA CHUO KIKUU TEOFILO KISANJI WALIUNGANA NA WANAFUNZI WENZAO WA KIISLAMU WA VYUO VIKUU VYA MKOA WA MBEYA (SAUT, MZUMBE, MUST, MMTC, MATI-IGURUSI, CDTI, TIA, TUMAINI UNIVERSITY, ST AGGREY, CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA CHA TANZANIA, N.K.)  KATIKA MAHAFALI YA KUWAAGA KAKA NA DADA ZAO AMBAO WANATARIJIA KUMALIZA MASOMO YAO MUDA SIO MREFU UJAO. MAHAFALI ILIFANYIKA KATIKA CHUO KIKUU SAUT, MBEYA.


WANAJUMUIYA WA TAMSYA MBEYA WAKIWA KATIKA MAHAFALI YA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU.

MAHAFALI ILIKUWA CHINI YA USIMAMIZI WA JUMUIYA YA WANAFUNZI NA VIJANA WA KIISLAMU TANZANIA (TAMSYA) MKOA WA MBEYA.
KULIKUWA NA HARAKATI MBALIMBALI ZA KIDINI IKIWEMO KUWAUSIA VIJANA WA KIISLAMU KUHUSU UJASIRIAMALI NA UMUHIMU WA KUJIAJIRI, UMUHIMU WA NDOA, UMUHIMU WA KUITUMIA ELIMU NA NYADHIFA MBALIMBALI KATIKA KUUPELEKA MBELE UISLAMU PAMOJA NA JINSI YA KUISHI KATIKA MAADILI YA KIISLAMU.


MH. MGENI RASMI, SHEIKH DUURU AKITOA MAWAIDHA YA KUWAUSIA VIJANA JINSI YA KUISHI MAISHA YA USILAMU PAMOJA NA KUITUMIA ELIMU YAO KWA MASLAHI YA DINI.
 
DR. SULE AKITOA MAWAIDHA NA KUFAFANUA UMUHIMU WA ELIMU KATIKA UISLAMU KWA MUJIBU WA QURANI NA SUNNAH.

PIA KULIKUWA NA USOMAJI WA RISALA  AMBAYO ILISOMWA MBELE YA MBENI RASMI NA BAADAE KUKABIDHIWA MGENI RASMI KAMA ILIVYO KAWAIDA. RISALA ILISOMWA NA ALIEKUWA AMIR WA MSATEKU AMBAE PIA ALIKUWA NI AMIR WA IDARA YA ELIMU, DAAAWA NA MAADILI TAMSYA, USTADH IMANI SALEH.
 
USTADH IMANI SALEH AKISOMA RISALA YA WANAJUMUIYA YA TAMSYA.


PIA KULIKUWA NA ZOEZI LA UGAWAJI WA VYETI KWA WANAFUNZI WANAOKARIBIA KUHITIMU MASOMO YAO, ZOEZI HILI LILIENDESHWA NA MGENI RASMI SHEIKH DUURU KUTOKA TAASISI YA DHIL-NNURAYN.
    
    
WANAFUNZI WAHITIMU NA WANAJUMUIYA YA TAMSYA NA MSATEKU WAKIKABIDHIWA VYETI VYAO VYA USHIRIKI NA MGENI RASMI SHEIKH DUUR KUTOKA TAASISI YA DHIL-NNUURAYN.


PIA KULIKUWA NA ZOEZI LA KUPIGA PICHA ZA PAMOJA ZA WANAJUMUIYA YA MSATEKU KWA AJILI YA UKUMBUSHO, PAMOJA NA KUWAAGA NA KUONESHA UPENDO KWA KAKA NA DADA ZAO WANAOTARAJIA KUONDOKA CHUONI BAADA YA KUMALIZA MASOMO YAO KATIKA SIKU CHACHE ZIJAZO.

 
             
PICHA ZA PAMOJA ZA WANAJUMUIYA YA MSATEKU ZILIZOPIGWA SIKU YA MAHAFALI YA TAMSYA MKOA WA MBEYA (2017). PICHA ZINAJUMUISHA WAHITIMU PAMOJA NA NDUGU ZAO WANAOENDELEA NA MASOMO.



UONGOZI WA JUMUIYA YA WANAFUNZI CHUO KIKUU TEOFILO KISANJI (MSATEKU, MBEYA) TUNAPENDA KUTOA SHUKURANI ZETU ZA DHATI KWA WATU WOTE WALIOSHIRIKI KATIKA MAHAFALI YA KUWAAGA KAKA NA DADA ZETU WANAOMALIZA MASOMO YAO, HATUNA CHA KUWALIPA ILA ALLAH (SW) ATAWALIPA KWA WEMA WAO WALIOUFANYA.
PIA TUNAWAPONGEZA KAKA NA DADA ZETU WANAOMALIZA MASOMO YAO, NA TUNAMUOMBA ALLAH (SW) AWAJAALIE KILA LA KHERI KATIKA MAISHA YAO BAADA YA MASOMO.
PIA TUNAMUOMBA ALLAH (SW) ATUJAALIE SIE SOTE AMBAO BADO TUNAENDELEA NA MASOMO TUENDELEE KWA SALAMA HADI KUFIKIA MWISHO TUMALIZE KWA SALAMA KWA UWEZO WAKE.
TUNAAMINI DINI YETU NDIYO ILIOTUUNGANISHA NA KUTUFANYA WAMOJA NA KUSHIRIKIANA KATIKA MAMBO YETU MBALIMBALI. MUNGU AJAALIE USHIRIKIANO NA UMOJA HUU UENDELEE KWA KIZAZI NA KIZAZI ILI KUUPA NGUVU UISLAMU.   AAAAMIIN.


WABILLAHI-TTAUFIQ

Saturday, 6 May 2017

MAANDALIZI YA KUUPOKEA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

  Tokeo la picha la WELCOME ramadhan 2017
Asslaamu alaykum warahmatu llahi wabarakaatuh;
Shukurani zote anastahiki Allah, na rehema na amani ziwe juu ya Mtume Muhammad.
Siku zote inatakiwa muislam asiwe mwenye kuzembea katika mambo mbali mbali yenye manufaa, khususani misimu ya utiifu kama vile Ramadhani. Bali inatakiwa awe wa mwanzo katika twa’a hizo na awe ni mwenye kushindana na kuhakikisha ya kwamba hakuna anaye mpita.
قال الله تعالي:( وَفِي ذَلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ)
المطففين:26
 Anasema Allah ndani ya kitabu chake kitukufu:
(Na katika hayo {mambo ya kheri} washindanie wenye kushindana). 
Suurat Al Mutwafifiin: 26
Imepita miezi, mawiki na masiku na hivi sasa umekaribia Mwezi wa Qur‘an, mwezi wa Baraka, mwezi wa ibada za usiku, mwezi wa kukubaliwa dua za waumini. Ewe Allah tufikishe Ramadhani!

Maswahaba walilelewa  na madrasa ya Mtume wakihisi hisia hizi za kuwa na shauku ya kuufikia mwezi wa fadhila, wakiishi na dua hii "Ewe Allah tufikishe Ramadhaan!"
Wakawa wakimuomba Allah awafikishe Ramadhani kabla ya miezi sita, na miezi sita mingine wakimuomba Allah akubali ibada zao.
Bila shaka hisia hizi na hali hii haikujengeka kwa Maswahaba isipokuwa kwa kujua fadhila za mwezi huu, na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Je ili tuweze kuupatia haki  mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tunatakiwa tufanyaje?
MAANDALIZI   YA MWEZI WA RAMADHANI:
Bila shaka shughuli yoyote ile huwezi kuifanya vizuri isipokuwa mpaka uwe na utaalam nayo na umeifanyia mazoezi. Tuchukulie mfano michezo, iwapo kama timu itakuwa na mechi basi hutenga muda maalumu kwa ajili ya mazoezi ili kujiweka fiti na mechi hiyo. Licha ya kwamba wana utaalamu na mpira lakini yawapasa wafanye mazoezi ili waweze zimudu pirika za uwanjani.
Vile vile ibaada mbali mbali ikiwemo funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani inahitaji ujuzi na maandalizi, ili tuweze  kuzikusanya fadhila mbali mbali zilizomo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ikiwemo kufutiwa madhambi, kukubaliwa ibaada hiyo ya funga na mengineyo.
Maandalizi hayo ni:
1. Kumuomba Allah Atufikishe Ramadhani
Kukithirisha kumuomba Allah atufikishe  katika mwezi wa ramadhani "Ewe Allah tufikishe Ramadhani":
Masiku haya ambayo tumeukaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani inatubidi tuzidishe sana kumuomba Allah atufikishe ramadhani.Kwani kufikishwa ramadhaani ni moja ya neema za Allah.Watu wengi watamani kufikkishwa mwezi mtukufu wa ramadhani lakini si kila mmoja  anaye tamani ataufikia.Kuna baadhi ya watu tulikuwa nao ramadhani iliyo pita lakini mpaka hivi sasa hatupo nao tena.Kwa hiyo sie tulio ruzukiwa uhai mpaka hivi sasa yatubidi tujitahidi kumuomba Allah atufikishe mwezi huu mtukufu wa ramadhani mwezi wa fadhila"Ewe Allah tufikishe ramadhani".
2. Kukithirisha kufunga katika mwezi wa shaabani:
Ni sunna kukithirisha swaumu katika mwezi wa shaabani kwa ajili ya kuiweka sawa nafsi kwa ajili ya kuupokea mwezi wa ramadhani.
Na hii ndio ilikuwa  hali ya mtume,kama anavyo simulia Ummu al mu-uminiina Aisha radhi za Allah ziwe juu yake   
(مَا رَأَيْتُ رَسُوْلَ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَ سَلَّمَ اسْتَكْمَلَ صِيَامَ شَهْرٍ قَطُّ إِلَّا رَمَضَانَ وَ مَا رَأَيْتَهُ فِيْ شَهْرٍ أَكْثَرَ صِيَاما مِنْهُ فِيْ شَعْبَانَ) 
رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
(Sikumuona Mtume anakamilisha swaumu mwezi mzima isipokuwa Ramadhani. Na sikumuona anakithirisha funga katika miezi kama alivyo kuwa akikithirisha kufunga katika mwezi wa Sha'baani)
Hadithi imepokelewa na Bukhari.
Kwa hiyo yapendezwa kuanza kufunga tokea mwanzo mwa mwezi wa Sha’aban, vile vile siku tatu katika mwezi; yaani ayyaamul baidh (Siku za tarehe13,14 na15 za kalenda ya Hijri) Vile vile siku ya Jumatatu na Alkhamis.
NB: Haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani
 عَنْ أَبِىْ هُرَيْرَةَ رَضِىَ الْلَّهُ عَنْهُ قَالَ:قَالَ رَسُوْلُ الْلَّهِ صَلَّىَ الْلَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:(لَا تُقَدِّمُوا رَمَضَانَ بِصَوْمِ يَوْمٍ وَلَا يَوْمَيْنِ إِلَّا رَجُلٌ كَانَ يَصُوْمُ صَوْما فَلْيَصُمْهُ) 
رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Imesimuliwa kutoka kwa Abu Huraira radhi za Allah ziwe juu yake kasema: Kasema Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake (Msitangulize Ramadhani kwa kufunga siku au siku mbili, isipokuwa kwa yule aliye kuwa akifunga kabla yake basi afunge) 
Hadithi imepokelewa na Muslim.
Yaani haitakiwi kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhani isipokuwa kwa yule aliyekuwa akifunga kabla. Mfano kwa yule aliyekuwa akifunga siku ya Jumatatu na Alkhamisi. Basi   ikidondokea moja ya hizo siku kabla ya Ramadhani  kwa siku moja au mbili hakuna tatizo kwa mtu huyu kufunga. Au kwa yule mtu aliye panga kufunga mwezi wa shaabani karibia wote kama alivyo kuwa akifanya mtume basi hakuna tatizo. Au kwa mtu aliyekuwa kajizoesha kufunga siku na kufuturu siku basi hakuna tatizo kwake kufunga pia.
Vile vile haitakiwi kufunga siku ya shaka. Na siku ya shaka ni siku ya thelathini ya mwezi wa shaabani ikiwa usiku wake ulikuwa ni wenye mawingu mengi kiasi kwamba ikawa hawezekani kujua kama kuna mwezi au hapana.Imeitwa siku ya shaka kwa sababu katika hali hiyo ya mawingu tunakuwa na shaka je mwezi umeonekana au hauja onekana?
Wanazuoni wametofautiana kuhusiana na katazo la kufunga siku hii ya shaka. Je ni katazo linalo fidisha uharamu wa kufunga siku hii au ni katazo linalo fidisha karaha (yaani yachukiwa)kwa hiyo ni bora zaidi mtu asifunge?
Rai yenye nguvu juu ya suala hili ni kwamba katazo hili linafidisha uharamu kufunga siku hii kama inavyo onekana wazi katika hadithi za Mtume (rehma na amani juu yake)
3. Kuishi na Qur ani:
Yatakiwa kujitahidi katika kusoma Qur ani angalau juzu moja kwa siku, ili mpaka unaisha mwezi wa shaabani unakua ushakhitimisha Qur ani japo mara moja. Vile vile yatakiwa kutenga muda maalumu kwa ajili ya kusoma na kuzingatia aya mbali mbali katika Qur ani na wala si kutosheka kwa kuisoma haraka haraka tu.
4. Qiyamu llayli:
Yatakiwa kujitahidi kuswali  ibaada za usiku tahajudi na witri; japo raakaa mbili tahajudi na rakaa moja witri. Swali rakaa mbili kwa mazingatio. Kumbuka swala ni mawasiliano kati ya mja na Mola wake. Wakati wa kuswali hisi ya kwamba unazungumza na Allah na anakuona na kukusikia. Soma suurat al Faatiha na sura baada yake kwa mazingatio na utulivu wa hali ya juu, kwa kufanya hivyo utahisi radha ya ibada isiyo sifika na kuhisi furaha ya maisha ya kweli. Kwani furaha ya maisha ya kweli inapatikana katika kumtii Allah sub-hanahu wata’ala na kukithirisha ibaada mbali mbali ikiwemo kuswali na ibaada za usiku. Na yule atakaye hisi ya kwamba kumtii Allah na kutekeleza ibaada mbali mbali  ni kujibana na kuto yafaidi maisha basi dhana yake hiyo itakuwa ni potofu.
5. Kujifunza hukumu zinazo husiana na Ramadhani:
Inatakiwa muislamu amuambudu Allah ‘azza wa jall kwa elimu au ujuzi, kwani kujua hukumu za faradhi mbali mbali ambazo Allah ta’ala kazifaradhisha kwa wanaadamu ni lazima kwa kila muislamu. Na katika faradhi hizo ni faradhi ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa hiyo yatakiwa kujua  hukumu na mas’ala mbali mbali yanayo husiana na funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ili funga zetu ziwe sahihi na ziweze kubaliwa. Kwa hiyo yatupasa kusoma vitabu mbali mbali vinavyo husiana na funga ya Ramadhani na kuwauliza wenye elimu katika yale mambo tunayo tatizwa nayo.
Anasema mwenyezi Mungu mtukufu ndani ya Qur ani
فَاسْأَلوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِنْ كُنْتُمْ لا تَعْلَمُونَ))
الأنبياء :7
(Basi waulizeni wenye elimu ikiwa nyinyi hamjui.)
Al anbiyaa:7
6.  Kuizoesha nafsi kwa kupunguza baadhi ya vyakula:
Inatakiwa ujizoeshe kuacha baadhi ya vyakula licha ya kwamba wavipenda ili nafsi yako itakapo fika Ramadhani iwe ishazoea hali ya kuacha baadhi ya mambo, hali itakayo pelekea kufunga Ramadhani kiurahisi. Yatakiwa ujitahidi kuipa dunia mgongo (Azzuhdi) kiasi kwamba mwezi wa shaabani kwako uwe una tofauti kiasi na miezi mingine katika vyakula, vinywaji mavazi na mengineyo. Mfano mzuri katika hili ni wale ambao huumwa na vichwa kwa sababu ya kukosa chai asubuhi, basi inafaa kuanza kujizowesha kukosa kunywa chai hata kabla ya mfungo wa Ramadhani ili ikifika Ramadhani jambo hili lisikupe taabu. 
7. Mazoezi ya ulimi:
Yatakiwa ujizoeshe kusema ukweli na kuachana na uongo, usengenyaji na ufitinishaji. Kwani mambo haya hayatakiwi yafanywe na muislamu yoyote na kwa mfungaji  basi makatazo yake ni ya hali ya juu. Haitakiwi mfungaji awe ni mwenye kudanganya kusengenya na kufitinisha watu.
قَالَ الرَسُوْلُ الله صَلَّى الله عَلَيْهِ وََسَلَّم: "مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّوْرِ وَالعََمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِله حَاجَةٌ فِيْ أَنْ يَدَعَ طعَامَهُ وَشَرَابَهُ" (رواه البخاري والترمذي وأبو داود وابن ماجه وأحمد)
Imetokana na Abu Hurairah (Radhi za Allaah ziwe juu yake), Amesema Mtume rehma za Allaah na amani zimshukie): “Yoyote ambaye hatoacha kauli za uwongo (chafu) pamoja na matendo, basi Allaah hana yaja ya mtu huyu kuacha kula na kunywa. (Imepokelewa na Bukhari, MuslimAbu Dawud, Ibn Majah na Ahmad)

Hadithi hii itatuthibitishia kwamba ulimi mchafu ni tosha kuwa sababu ya kutokubali kwa funga ya mfungaji.
8. Kuihesabu nafsi:  
Ni bora kila mwisho wa siku ukakaa na kuihesabu nafsi yako umefanya madhambi mangapi na kumtubia Allah na kuahidi ya kwamba huto rudia tena, na kukumbuka adhabu ya moto, je mwili wako upo tayari kuishi motoni? Bila shaka hii pia itakusaidia  katika kutekeleza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa ukamilifu. Kwani funga ya Ramadhani si kujizuia na vyakula vinywaji na yale yenye kufuturusha, bali ni funga ya mauvo pia. Lengo la funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kuwafanya watu wawe wachamungu. Na uchamungu ni kufuata maamrisho ya Allah na kuachana na makatazo yake. 
Bila shaka maandalizi haya iwapo kama tutayatekeleza  kiukamilifu,  basi ya yanatosha kuwa sababu kuufunga mwezi wa Ramadhani kiukamilifu,   kiurahisi na kuhisi thamani ya Ramadhani na kutamani laiti mwaka wote ungekuwa ni Ramadhani.
Ewe Allah tufikishe Ramadhani na ukubali ibada zetu, hakika Wewe ni Msikivu, Mjuzi wa yote na juu ya kila jambo ni Muweza.

KUIPOKEA RAMADHANI KWA KUVUNJA JUNGU NI MAASI

 Tokeo la picha la ramadhan 2017
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
Assalaamu Alaykum Warahmatullah!
Ni baada ya siku chache tu kwa msaada wake Allah Karim utakuwa unapumua na kuishi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi ambao huwapa waislamu fursa ya kuitekeleza mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, swaumu ya Ramadhani. Katika kuuheshimu, kuutukuza na kuuenzi mwezi huu mtukufu.

Naam, Ramadhani hiyo mlangoni mwako inabisha hodi. Wewe kama muislamu umejiandaje kuupokea mwezi wako huu mtukufu? Je, wewe ni mmoja wa wale wanaoupokea mwezi wa Ramadhani kwa kile kinachojulikana kama VUNJA JUNGU?

Hebu na tujiulize kwa pamoja, tulivunjao hilo jungu mwaka hata mwaka na wale tusiolivunja, vunja jungu ni nini khasa? Bila ya shaka mtakubaliana nasi kwamba vunja jungu kama litafsirikanavyo kutokana na matendo yatendwayo na wavunja jungu katika kulivunja kwao hilo jungu. Ni mkono wa kwaheri unaopungwa kwa maasi mbalimbali kwa ajili ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wavunja jungu huitumia fursa ya zile siku mbili tatu kabla ya kuandama kwa mwezi mwandamo unaoashiria kuanza kwa funga tukufu ya Ramadhani.

Kuogelea na kupiga mbizi maradufu katika maasi waliyokuwa wakiishi nayo katika kipindi cha ile miezi kumi na moja nje ya Ramadhani. Kwa hivyo basi, vunja jungu kwa mlevi ni kulewa sana kwani hataipata fursa hiyo tena ila baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.

Vunja jungu kwa mzinifu ni kuzini sana na kutengana na kimada wake kuipisha Ramadhani, kisha mchezo uendelee baada ya Ramadhani. Vunja jungu kwa mpenzi wa muziki ni kukesha katika kumbi za starehe akicheza na kunywa kufidia ile fursa atakayoikosa kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu. Mbele za watu hawa Ramadhani ni mithili ya gereza/kifungo kinachowaondolea na kuwanyang`anya uhuru wa kuishi kama wapendavyo kwa kufuata matashi na matamanio ya nafsi zao.

Hawa wanasahau kwamba wanawajibika kuishi kwa mujibu wa muongozo wa Mola Muumba wao na sio kwa kuongozwa na matashi yao! Kwa ujumla vunja jungu ni kushindana katika aina mbalimbali za maasi kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao hautoi uwanja wa maasi hayo kwa mijibu wa fikra zao potofu. Kwa nini tunasema kwa mujibu wa fikra zao potofu, hilo linatokana na ukweli kwamba hakuna kibali wala uhalali wa kufanya maasi na mtu kuishi kama apendavyo nje ya Ramadhani.

Ikiwa vunja jungu linaashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuonyesha kufilisika kiimani kwa huyo mvunja jungu. Kwani muumini wa kweli hawezi kuvunja jungu, kwa kuwa anatambua kwamba kufanya hivyo ni kumuasi Allah Mola Muumba wake. Kwa muumini wa kweli kujiepusha na maasi na kumtii Mola wake ni zoezi linaloyatawala maisha yake yote. Bila ya kuangalia kuwa huu ni mwezi wa Ramadhani au ni nje ya Ramadhani. Kuagana na maasi eti kwa sababu tu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kisha kuyarejea tena baada ya kumalizika kwake.

Huo tukubali au tukatae ni UDHAIFU WA IMANI na si vinginevyo. Kwani huyo Mola wa Ramadhani unayeacha maasi ndani yake kwa ajili yake, ndiye Mola wa hiyo miezi mingine unayojihalalishia maasi ndani yake. Amri ya kumtii Mola wako kwa kuyatekeleza yote aliyokuamrisha na kuyaacha yote aliyokukataza inauhusu mwezi wa Ramadhani na baki ya miezi mingine isiyo Ramadhani.

Kumuabudu Mola wako ndani ya Ramadhani tu ni kujiuundia utaratibu wa ibada kinyume na ule aliokupangia Allah Mola Muumba wako. Elewa kufanya kwako hivi ni sawa na kusema kuwa utaratibu wa ibada aliokuwekea Mola wako aliye mjuzi wa manufaa na maslahi yako ama haufai au umepitwa na wakati. Na kwamba wewe kama kiumbe unaweza kujiundia utaratibu utakaokudhaminia manufaa na mafanikio katika ulimwengu wako huu na ule ujao. Elewa kwa mtindo na mtaji wako huo siku ya kiyama Allah atakuambia ujilipe wewe mwenyewe kwa kuwa yeye hakukuamrisha kufanya ibada kwa utaratibu huu unaokwenda nao sasa.

Ewe ndugu mpenzi wee! Elewa na ufahamu fika kwamba Ramadhani ipokelewayo na kukaribishwa na vunja jungu haitakuwa na athari yo yote kwako wewe ambaye ndiwe mlengwa wa Ramadhani na wala sio Mola wako. Kwako Ramadhani haitakuwa ila mithili ya kujenga nyumba angani bila ya kuwa na msingi imara uliokita ardhini.

Ewe ndugu mpenzi mvunja jungu, utaendelea kulivunja hilo jungu na kumuasi Mola wako mpaka lini?! Hebu jiulize, nini utakuwa mwisho wa huku kuvunja jungu kwako?! Tangu umeanza kuvunja jungu na bila shaka ni jungu la maasi umepata na kuvuna nini?! Ndugu mpenzi hebu ihurumie nafsi yako kwa kuitegea sikio la usikivu kauli hii tukufu ya Mola wako: "ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE (vile vile)…" [41:46]

Aya inakuongoza kutambua kwamba unapovunja jungu, hufanyi hivyo ila ni kwa hilaki na maangamivu ya nafsi yako wewe mwenyewe leo hapa duniani na kesho kule akhera. Ambapo utapewa daftari la amali zako uikute na vunja jungu yako, hapo ndipo utasema: "…OLE WETU! NAMNA GANI MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYA YAMEHUDHURIA HAPO; NA MOLA WAKO HAMDHULUMU YO YOTE". [18:49]

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: "Jibril alinijia na akaniambia: Ewe Muhammad! Ishi utakavyoishi, hakika wewe ni mwenye kufa. Na penda ukipendacho hakika utatengana nacho, na tenda ulitakalo hakika utalipwa kwalo…" Al-Baihaqiy Elewa ewe ndugu mpenzi ukiwa mwana kuelewa, elewa kwamba kwa mujibu wa hadithi hii:-
Vunja jungu yako ina mwisho wake ambao ni kufa kunakoashiria mwanzo wa safari ngumu ya kuhudhurishwa mbele ya Mola wako. Hii ndiyo siku anayoitaja Mola wako kwa kauli yake tukufu: "NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA". [2:281]

Lewa sana kwani pesa ni zako,zini sana na endelea kuvunja jungu, lakini tambua kuwa iko siku moja utalipwa kwa yote uliyoyatenda hapa duniani: "BASI ANAYEFANYA WEMA (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE. NA ANAYEFANYA UOVU (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE". [99:7-8]

Ewe mvunja jungu wee! Hebu waidhika na sehemu hii ya kauli ya swahaba wa Mtume;Sayyidna Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi: "Ewe mtenda dhambi wee! Usijiaminishe na matokeo ya dhambi yako na tambua kwamba kiifuatiacho dhambi hiyo ni kikubwa kuliko dhambi yenyewe.

Kwani kule kutokuwaonea kwako haya malaika walioko kuliani na kushotoni kwako wakati unapofanya dhambi, hakupungui kuwa ni dhambi. Na kicheko chako wakati unatenda dhambi na ilhali hujui Allah atakufanya nini, ni kikubwa zaidi kuliko hiyo dhambi uitendayo.

Na kuichelea kwako dhambi unapofanikiwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko hiyo dhambi yenyewe. Na kuihuzunikia kwako dhambi kwa kushindwa kuitenda, ni kukubwa zaidi kuliko dhambi husika. Haya mpenzi mvunja jungu, ikiwa mpaka hapa bado hujawaaidhika na ukaacha kulivunja hilo jungu, hebu zidi kutega sikio:

Mtu mmoja alimwambia Sufyaan Thauriy-Allah amuwiye radhi-nipe nasaha ambazo nikizifanyia kazi sitathubutu kumuasi Allah. Sufyaan akamwambia: Yakumbuke mambo matano:
Je, inastahiki kwako kumuasi Allah na ilhali yeye ndiye anayekuruzuku?
Je, unadhani kuwa wewe unamuasi Allah na ilhali yeye anakuona?
Je, unaweza kumuasi Allah nje ya ufalme/milki yake?
Je, unaweza kuyaakhirisha mauti yakikujia?
Je, siku ya kiyama utakuwa una uwezo wa kujiondoshea adhabu?
Yule mtu akajibu: Siwezi lo lote katika hayo. Sufyaan akamwambia: Basi vipi unathubutu kumuasi yule anayekuruzuku, anakuona, nawe uko katika milki yake, akakuandikia mauti na wala huwezi kuizuia adhabu yake isikufike? Akasema mtu yule: Wallah sitamuasi muda wa uhai wangu.

Hebu nawe mvunja jungu, jiulize maswali matano hayo halafu ndio uamue ama kulivunja jungu au kutokulivunja. Kumbuka ewe ndugu muislamu kwamba:-
Kuvunja jungu ni kumuasi Allah na Mtume wake: "NA ANAYEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, NA KUIRUKA MIPAKA YAKE (Allah) ATAMUINGIZA MOTONI. HUMO ATAKAA MILELE NA ATAPATA ADHABU ZIFEDHEHESHAZO". [4:14]

Kuvunja jungu ni kuudhihaki mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuudhihaki mwezi huu hakumaanishi kingine zaidi ya kuidhihaki Qur-ani Tukufu. Nako huku kuidhihaki Qur-ani, hakika si vinginevyo ila ni kumdhihaki aliyeshushiwa Qur-ani Mtume. Na hakuna anayethubutu kupinga kwamba kumdhihaki Bwana Mtume ni kumdhihaki Allah akiyemtuma. Na huko kumdhihaki Allah ni ukafiri tu na si vinginevyo: "AMA WALE WALIOKUFURU, NITAWAADHIBU ADHABU KALI KATIKA DUNIA NA AKHERA, WALA HAWATAPATA WASAIDIZI WA KUWASAIDIA". [3:56] Vunja jungu ni khadaa na ghururi za dunia. Uovu basi si huko kukhadaika, bali ni kushikilia kukhadaika baada ya kutanabahishwa. Wasalaamu Alaykum Warahmatullah.
_________________
Jazaakumullah
MWISHO

Wednesday, 11 January 2017

VIPI MWANAFUNZI WA KIISLAMU ANATAKIWA AWE KATIKA SAFARI YA KUTAFUTA ELIMU

Kila msomi azingatie Ilani ya Elimu ya ‘Jabal Hirah’
Lengo lisiwe stashahada, astashahada, shahada ya msingi, Uzamivu na Uzamili tu pekee.
Je, Msomi wa Viwango vya juu ni aibu kuitwa Ustaadh?



Safari ya kila mwanafunzi wa Kiislamu kutoka nyumbani kwake kwenda shule/Chuo lazima iwe sawa na ile safari ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, kutoka nyumbani kwake kwenda pangoni, Jabal Hirah.

Kama ambavyo Mtume aliambiwa “Soma” kwa Jina la Mola wako basi kila mwanafunzi wa Kiislamu anatakiwa asome hivyo. Mwenyezi Mungu alimpa changamoto Mtume Wake kwa sura ya mwongozo.

Kwamba kila atakachokisoma akisome kwa ajili ya Mola wake. “Soma kwa Jina la Mola wako aliyeumba.” Kipande hiki cha aya za Mwanzo za Qur’an kinabeba maana kamili ya kusoma.

Aya hiyo ina maana kuwa chochote utakachokutana nacho katika kutafuta elimu kimeumbwa na Mwenyezi Mungu. Hii maana yake, kimsingi, ni kwamba vile vinavyosomwa ni matokeo ya kazi ya Mwenyezi Mungu.

Kwa ajili ya kutoa changamoto, Mwenyezi Mungu kaanza na baiolojia ya mwanadamu mwenyewe anayetakiwa kusoma, “Amemuumba mwanadamu kwa pande la damu.”

Mwenyezi Mungu hakutaka kuanza kwa kumpeleka mbali mja wake anayetafuta elimu bali kaanza na umbile lake mwenyewe. Aya hii inawasuta wale waliofanya jitihada za kutenganisha elimu inayoitwa ya dunia na ile ya dini.

Jitihada hizo mbaya zilikuwa na hila ya kumtenga Mungu na ile inayoitwa ‘elimu dunia’. Kwamba watu wavisome vilivyoumbwa bila kumjua aliyeviumba. Ulimwengu umezugwa na kuzugika kwamba Mungu atafutwe zaidi katika imani ya kiroho, na si katika maumbile aliyoyaumba.

Si ukweli wa kuficha kuwa ulimwengu umeachwa kwenye upofu wa kutomuona Mungu kwa hila iliyofanywa na Wapinzani wa Mungu. Mungu amebaki kama “dhana tu ya kiroho” ambapo kumwamini au kutomwamini kama yupo ni hiyari ya nafsi na si hitajio la kiakili.

Profesa wa Baiolojia hamuoni Mungu katika fani aliyosomea bali anamtafuta rohoni zaidi kwa mawaidha ya Msikitini ya Sheikh ambaye upeo wake juu ya maumbile si mkubwa kama ule wa Profesa.

Mwenyezi Mungu aliwahi mapema kutaka waja Wake wasome kwa Jina Lake, na kisha akaweka wazi mapema kuwa Yeye ndiye aliyeumba. Ilani hiyo ya Elimu iliukusanya mfumo mzima wa elimu ndani ya tauhiid.

Mosi, kulisoma pande la damu sio kusoma Fiqh wala thanawi bali ni kusoma sayansi ya Baiolojia ambayo, kwa hila za wapinzani wa Mwenyezi Mungu, imeitwa ‘elimu dunia’ ili eti msomaji wa sayansi hiyo asilihusishe somo hilo na dini.

Asome tu na kubobea, akikusanya vyeti vya kitaaluma, stashahada, astashahada, shahada ya msingi, shahada ya uzamili na uzamivu pamoja na kupewa heshima lukuki za kitaaluma.

Kazi nzuri yenye mshahara mzuri ndiyo lengo la msomi huyu. Gari nzuri ya kutembelea, nyumba nzuri ya kuishi, maisha mazuri ya kula na kunywa ndiyo yanayoonesha umuhimu wa jitihada alizozifanya za kutafuta elimu.

Kama hicho ndicho kilele cha jitihada za kutafuta elimu basi akili ya binadamu itakuwa imeishia pale ilipoishia ya mnyama napo ni pale pa kutafuta kula na kunywa.

Ilani ya Elimu iliyotolewa Jabal Hira inatupa mtazamo tofauti kabisa na huo. Mwanafunzi au Msomi wa Kiislamu lazima aizingatie Ilani hii. Kwa kuizingatia Ilani hii, kila somo linaingia na kufungiwa ndani ya dhana ya Tauhiid.

Wakati Qur’an ikitoa changamoto ya matumizi ya akili, na ikitoa dondoo za kisayansi katika aya mbalimbali ili kumkumbusha mwanadamu, msomi anapaswa kuielekeza akili yake katika fani yake, na kuisoma Qur’an kama Ilani ya Elimu yake.

Nguvu ya Tauhiid itakayojengeka kwa kuunganisha Aya za Qur’an na fani mbalimali za elimu itakuwa kubwa mno. Mwenyezi Mungu ataonekana kwenye Baiolojia, Kemia, Fizikia, Jiografia, Jiolojia, Hisabati na kadhalika.

Imani itakayojengeka hapa itakuwa ni ya yakini, sio ya mashaka-mashaka. Ibada itakayofanyika kwa msingi wa elimu hii itakuwa ni ibada ya hakika, sio ya mazoea na ya mkumbo.

Mwanafunzi atakayesoma kwa mtazamo huu hatahitaji kiboko cha kumswaga aende Msikitini, na moyo hautamruhusu kukwepa Swala. Mwanafunzi atakayesoma kwa mtazamo huu hatakuwa mtumishi wa tumbo lake, bali atakuwa Mtumishi wa Mola wake.

Akili ya msomi wa sampuli hii haitaishia kuijua falsafa ya fani yake bali itasumbuliwa na ishara za Muumba. Dhikiri au kumkumbuka Mwenyezi Mungu ambako huonekana kama ni utamaduni wa kiroho ndani ya Majumba ya Ibada nyakati za swala itachukua sehemu kubwa kichwani na moyoni mwa msomi huyu.

Kila wakati atatawaliwa na wingi wa utukuzo na shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kazi aliyoifanya, kuanzia akili inayomwezesha msomi kusoma kuja neema nyingine. Umbile lake mwenyewe kila siku na kila wakati litakuwa ishara mpya ya kumuona Muumba wake.

Anapovaa shati na kujitazama kwenye kioo, hatoishia kuona kuwa kapendeza bali ataona sanaa ya Mwenyezi Mungu katika umbo lake na mara moja ataisifu na kuitukuza Kazi ya Mola wake.

Msomi huyu hawezi kupitisha sekunde au dakika bila kulitafakari umbile lake, na umbile la Mbingu na Ardhi. Akijitazama mwenyewe au akiwatazama wanadamu wenziwe mara moja humuona Muumba wake.

Anapoyatazama macho yake mwenyewe au ya mwenziwe anayetazamana naye hutanabahi, ni Nani aliyeweka macho haya mawili yanayofanya kazi muhimu kwa ushirikiano wa ajabu na ubongo!

Kama anasomea sayansi ya macho basi ndio kabisa atatosheka na jicho tu kumuona Mola wake hata kabla ya kutazama neema nyingine. Macho anayosomea yatakuwa msingi wa tauhiid, na yatakuwa ishara ya kila siku ya kumuona Mola wake.

Kama anasomea kinywa basi atatosheka na mfumo wa kinywa kwa jinsi ulivyopangiliwa meno yenye kazi ya kukata na kutafuna, na atastaajabu, ni Nani huyu aliyekipangilia kinywa namna hii!

Kinywa anachokisomea na kubobea kwacho kitakuwa msingi wa tauhiid na ishara ya kila siku ya kumuona Mola wake. Kama anasomea fuvu la kichwa, basi atajiuliza wakati wote, ni Nani huyu aliyeweka fuvu gumu ili kuukinga ubongo ambao unahitaji kweli kukingwa?

Kwa nini ubongo umekuwa ndani, fuvu limekuwa nje, hebu ona madhara yanayotokea pale ubongo unapoathirika? Ni Nani huyu aliyeuwekea kinga muhimu ubongo? Laiti fuvu la kichwa lingekuwa laini na la kubonyea-bonyea, ubongo usingelikuwa salama hata kidogo.

Hivyo, kwa kuvuta tafakuri hii pale anaposomea fani yake, msomi wa mrengo huu, hubakiwa na jawabu la hakika kichwani mwake kuwa yeye na kile anachosomea ni matokeo ya kazi aliyofanya Mwenyezi Mungu.

Hivyo, fani yake ya fuvu la kichwa inakuwa msingi wa tauhiid. Moja kwa moja anamuona Mwenyezi Mungu katika elimu yake, na siyo kumtafuta kwenye mawaidha ya Sheikh.

Anayesomea jiografia husomea mzunguuko wa sayari, na huona umakini usio wa kawaida ambao tangu ulimwengu ulipoanza miaka dahari, sayari zimekuwa zikizunguuka kwa kasi bila ajali yoyote!

Kupatikana kwa usiku na mchana na mabadilikon ya majira ni matokeo ya mzunguuko huo. Msomi wa fani hii atakayezingatia Ilani ya Elimu ya Jabal Hirah muda wote atasumbuliwa na swali kichwani, ni Nani huyu aliyeumba mfumo wa sayari na kuuzunguusha kwa usalama ili kuleta mabadiliko ya nyakati, usiku na mchana na misimu ya masika, kiangazi, kipupwe na kadhalika?

Ni Nani aliyeumba Bahari yenye manufaa kwa wanadamu, na kitoweo cha samaki kinachokamilisha lishe yake? Ni Nani aliyeweka ekolojia ya mvuke wa maji unaoevukia angani kwa upepo wa miti kwa ajili ya kutengeneza barafu ambayo hatimaye huyeyuka na kuleta mvua ambayo ni muhimu kwa maisha ya viumbe vyote vya ardhini?

Bila maji, maisha yasingelikuwepo? Ni Nani huyu aliyeweka ekolojia hii muhimu? Msomi hapa atamuona Mungu kabla ya kwenda Msikitini. Yeye ndiye atakayemthibitisha Mungu kuliko Sheikh anayeamini kiroho zaidi.

Kumbukumbu ya Mungu itakuwa ya kudumu akilini mwake, na haitakuwa ile ya wakati wa swala pekee. Msomi wa Jiolojia naye ataitazama milima na kuona jinsi inavyoisaidia dunia isiyumbishewe na kasi ya mzunguuko wa dunia.

Bila milima, amani isingelikuwepo. Maisha yangelikuwa ya kutetemeshwa na kubidukabiduka wakati wote. Lakini vigingi vilivyowekwa kwa sura ya milima vinafanya kazi muhimu ya kuibakisha ardhi katika utulivu unaofanya watu waone kama vile hakuna mzunguuko wowote.

Mtu wa kawaida hupata tabu kuelewa pale anapoambiwa dunia inabimbilika kwa sababu mbona hatubimbiliki. Hii ni hisani kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo msomi wa jiolojia anapaswa kuiona na kuwafafanulia watu wasiojua ili kwa pamoja tuungane kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Jiografia ni somo la Kiislamu, na si somo la “kizungu”. Kuyasoma maumbile ya Mwenyezi Mungu kunamwakisi Muumba, hakumwakisi Mzungu. Ukisoma jiografia unamuona Mungu, sio Mzungu.

Mifano hiyo itoshe kuonesha athari za Ilani ya Elimu ya Jabar Hirah. Ilani hiyo haimfanyi msomi Muislamu aache kusoma kwa ajili ya Mola wake na badala yake ajiwekee lengo bandia la kusomea stashahada, astatashahada, shahada ya msingi, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu, na baadae kupata kazi nzuri basi!

Badala yake, Ilani hii ndiyo itakayotupatia Makhalifa wa kweli wa kusimamisha Ufalme wa Mwenyezi Mungu. Mapinduzi ya kiitikadi yatakuja yenyewe yakiwa ni matokeo ya athari za ilani hii ya Elimu.

Ilani hii ya elimu ndiyo itakayotupatia wasomi halisi wa Kiislamu katika kila fani. Mjumuiko wa fani hizi ndio unaojenga jamii ya wasomi wanaoweza kuendesha mambo ya dunia kwa kuzingatia maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Wimbo wa kusimamisha Uislamu, mwito wa Jihadi vyote haviwezi kupata matunda bila kutekeleza Ilani hiyo ya Elimu ya Jabal Hirah. Tunaweza kirahisi kuimba wimbo wa kusimamisha dola ya Kiislamu, na tunaweza kirahisi kuitisha jihadi lakini mwisho wa siku, wimbo hautachezeka, wala mwito hautatimia kama hatutapata Jamii ya watu waliosoma kwa Ilani hiyo.

Tunaposema Uislamu ni itikadi ya kimapinduzi basi maana yake ni kwamba kila eneo la maisha linahitaji wasomi wa mrengo wa Kiislamu. Huwezi kujenga Uchumi wa Kiislamu bila kusomesha wachumi kwa Ilani ya Jabal Hirah.

Tunapozungumzia kusimamisha Uislamu, na tunapozungumzia Jihadi, dira letu lazima liangaze mbali sana kwamba hatimaye tutakuwa watu wa aina gani wa kuendesha serikali, na tuna watu wa aina gani wa kupigana jihadi.

Kwa Uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa Malaika kutoka Mbinguni, Mtume angeliweza kusimamisha Uislamu siku ileile ya kwanza aliyopewa Wahyi Jabal Hirah.

Au angeliweza kupigana Jihad Maka badala ya kuhamia Madina. Lakini bado kulikuwa na kazi ya kuijenga jamii, kuwajenga watu wa kupigana Jihadi, kuwajenga watu wa kusimamisha Uislamu, na kuwajenga watu wa kutawala na kutumikia Dola ya Kiislamu.

Kwa nini Mtume aliyekuwa na Nguvu za Mwenyezi Mungu nyuma yake na msaada wa Malaika alihitaji miaka mingi kusimamisha Dola ya Kiislamu? Jihadi ni faradhi lakini ni matokeo ya jitihada za awali za kujenga jamii ya Kiislamu.

Kubwa kabisa katika jitihada hizo ni kusomesha watu elimu zote kwa kuzingatia Ilani ya Jabal Hirah. Tunahitaji diploma, digrii kwa kuzingatia ilani hiyo. Hapo ndipo dhana ya mapinduzi ya Kiislamu itakapotimia.

Kwa ujumla, Ilani hiyo ya Elimu ndiyo ya kuwakomboa Waislamu kifikra na kiitikadi. Itawatoa katika dhana potofu kuwa ‘ukisoma sana’ Chuo Kikuu hustahili kuitwa Sheikh au Ustaadh!

Itawajengea hali ya kujiamini kuwa uanataaluma hautenganishwi na usheikh wala uustaadh. Bali uanataaluma sahihi ni mchanganyiko wa yote hayo. Yeye huyo huyo awe Daktari, yeye huyo awe Profesa, yeye huyo huyo awe Sheikh na Ustaadh kwa maana ni msomi yuleyule anayesoma kwa Jina la Mola wake.

NAFASI NA UMUHIMU WA ELIMU KATIKA DINI YA UISLAMU


Nafasi ya elimu katika dini Tukufu ya Kiislamu

As-Salamu Alaykum 

Moja ya amali nzuri katika Uislamu ni kutafuta elimu. Katika Qur’ani Tukugu Mwenyezi Mungu ameanza kumhutubu mwanadamu kwa maneno ya “Kusoma”, “Elimu” na “Kitabu.” Hii ni kwa sababu elimu ni njia ya kufikia saada na ukamilifu wa mwanadamu. Mwanadamu kwa kutumia elimu, anaweza kuainisha mustakbali autakao yeye. Mara zote Mtume Mtukufu (saw) na masahaba zake, walikuwa wakihimiza sana kusoma. Katika mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu imenukuliwa kuwa, baada ya vita vya Badr kila mateka ambaye alikuwa akiwafundisha kusoma na kuandika wakazi 10 wa mji wa Madina, alikuwa akiachiliwa huru. Suala hilo ni ushahidi tosha na wa wazi juu ya uzingatiaji mkubwa wa dini ya Kiislamu na Mtume Muhammad (saw) kuhusiana na elimu na utafutaji wake kwa ujumla. Mtukufu huyo alikuwa akiipa umuhimu mkubwa kila aina ya elimu kama vile alivyomtaka mmoja wa masahaba zake kujifunza lugha ya Kisyriac. Mtume Mtukufu (saw) amepokelewa akisema, “Tafuteni elimu hata kama ni kutoka China.” Hadithi hiyo kama zilivyo hadithi nyinginezo, inasisitizia umuhimu wa elimu katika Uislamu. Sisitizo na ushawishi huo, kuhusiana na elimu, ndivyo vimewafanya Waislamu kutilia umuhimu na kufanya juhudi kubwa za kutafua elimu duniani. Mbali na hayo Waislamu walikuwa wakitarjumu kila athari yoyote ya kielimu waliyoipata. Kwa utaratibu huo, licha ya kwamba, Waislamu waliunda mfumo wa mahusiano kati ya tamaduni za Ugiriki, Urumi, Misri, India na nyinginezo, waliweza pia kuibua utamaduni na ustaarabu muhimu katika historia ya mwanadamu, uliokuja kufahamika kwa jina la “Utamaduni na Ustaarabu wa Kiislamu.”
************************************
Kwa mujibu wa mtazamo wa Waislamu, elimu na dini ni vitu viwili visivyotengana, bali ni vitu vinavyoenda sambamba. Kadhalika taaluma mbalimbali za kielimu kama vile fizikia, nyota, elimu ya ardhi, elimu ya tiba, hesabu na mithili ya hizo, zilikuwa zikifundishwa katika vituo vya kielimu vya Waislamu. Aidha mbali na hayo, Waislamu waliasisi maktaba kubwa tofauti katika vituo vya kielimu na kidini na hivyo kuifanya elimu na dini kuwa vitu viwili vinavyohitajiana. Hii ni katika hali ambayo uelewa finyu wa viongozi wa Kikristo kuhusiana na uhusiano wa dini na elimu, ulipelekea historia ya Ulaya kugawanyika katika zama mbili za kipindi cha imani na kipindi cha elimu, huku wakiifanya elimu kukabiliana na imani. Katika Karne za Kati, mitazamo ya kielimu na kifalsafa, ilikuwa ikitolewa tu na kanisa na hakuna msomi yeyote aliyekuwa na haki ya kutoa nadharia yake ya kielimu kinyume na mtazamo rasmi wa kanisa, kiasi kwamba, nadharia ya kielimu iliyokwenda kinyume na mtazamo wa kanisa, ilionekana kuwa ni sawa na kukufuru na kumpinga Mungu. Kwa msingi huo wasomi waliokuwa wakitoa mitazamo iliyopingana na mitazamo rasmi ya kanisa walikuwa wakifungwa jela, kuhukumiwa kifo au kuteketezwa motoni.
*************************************

Dini Tukufu ya Kiislamu iwe ni katika maandiko yake au kwa upande wa mwenendo wake wa kihistoria haina mkinzano wowote ule, bali tangu mwanzoni mwa kudhihiri kwake ilitoa amri ya watu kutafuta elimu, kiasi kwamba, sehemu kubwa ya aya na riwaya za kidini imezingatia zaidi suala la elimu na umuhimu wake na kubainisha thamani ya mtu aliye na elimu. Kwa hakika nafasi ya elimu katika Uislamu ni muhimu mno na ina daraja ya faradhi ya kidini. Hii ni kwa sababu hakuna mipaka katika kutafuta elimu. Kwa mtazamo wa Uislamu elimu zote ambazo zina faida kwa mwanadamu, zinapaswa kusomwa na watu. Kuhusiana na hilo Mtukufu Mtume (saw) anasema, “elimu ni zaidi ya kile ambacho kinaweza kuhesabika, basi chukua kile kilicho bora.” Kwa mujibu wa wa riwaya hiyo, Uislamu haukubana elimu katika fani fulani tu, bali umewataka wafuasi wake kujifunza na kutafuta elimu zote ambazo zina manufaa kwa mwanadamu. Kimsingi ni kuwa, Waislamu wanaamini kwamba, kadiri mtu anavyokuwa na elimu kubwa, ndivyo maarifa yake kwa Mwenyezi Mungu yanavyokuwa mengi. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa fikra ya Kiislamu, elimu na dini ni mambo mawili yanayoambatana kikamilifu. Katika Uislamu elimu yenye manufaa imesisitizwa sana. Aidha kwa mtazamo wa Uislamu, elimu haina maana ya elimu ya kidini au elimu ambayo ina manufaa kwa Akhera tu hapana, bali kusudio la elimu yenye manufaa ni elimu ambayo ina manufaa kwa mwanadamu kwa njia moja au nyingine, yawe ni ya kimaada au ya kimaanawi.
*****************************************
Katika aya ya 11 ya Surat al-Mujaadala, Mwenyezi Mungu anaelezea umuhimu wa elimu na daraja ya juu waliyonayo maulama na wasomi mbele ya watu wengine kwa kusema: "Mwenyezi Mungu anawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu."
Neno ‘Darajaat’ yaani daraja, lililotumika katika aya hii na lenye maana 'mutlaki' yaani bila kuainisha kiwango hasa cha daraja hiyo, katika lugha ya Qur'ani linabainisha adhama na ukubwa. Yaani kwa lugha nyingine ni daraja za juu. Katika kufasiri aya hii tukufu, Sahaba Abudhar al-Ghaffari amenukuliwa akisema kwamba, Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwambia: Ewe Abudhar, Mwenyezi Mungu, malaika na mitume wake wanampenda Twalibul-ilmi, yaani mtu anayetafuta elimu. Na elimu haipendwi ila na mtu mwenye saada, hivyo ni furaha gani atakayokuwa nayo mtu mwenye kutafuta elimu siku ya Kiama. Na mtu yeyote anayetoka nyumbani kwake kwa ajili ya kujifunza mlango mmoja wa elimu, basi Mwenyezi Mungu atamuandikia malipo kwa kila hatua atakayoipiga sawa na thawabu za mmoja wa mashahidi wa vita vya Badr. Na mtafutaji wa elimu ni kipenzi wa Mwenyezi Mungu na mtu yeyote atakayekuwa na mapenzi na elimu, basi pepo ni mali yake. Na atakuwa katika radhi za Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni na hatoondoka duniani isipokuwa atanyweshwa katika Haudh ya Kauthar. Kisha atakula matunda ya peponi na akiwa peponi atakuwa rafiki wa Hadhrati Khidhri (as).” Katika hadithi nyingine Mtume Mtukufu anasema: “Siku ya Kiama, wakati mtu mwenye elimu na mchaji-Mungu watakuwa kwenye Swiratw, yaani njia nyembamba, mchaji-Mungu ataambiwa, aingie peponi na afurahie matunda ya ibada yake aliyoifanya duniani. Na mtu mwenye elimu ataambiwa; bakia hapa na umuombee shufaa mtu au rafiki yeyote umtakaye, kwani kila yeyote utakayemuombea basi dua yako atakubaliwa. Hivyo yule mtu mwenye elimu atasimama katika kisimamo cha Mitume na kuwaombea marafiki na watu wake wa karibu ili wasamehewe dhambi zao. Kwani siku ya Kiama makundi matatu ndiyo yatakayokuwa na hadhi ya kufanya maombezi yaani shufaa, makundi hayo ni Mitume, wasomi na mashahidi.” Mwisho wa hadithi.
*****************************************
Katika hadithi za Ahlubayti wa Mtume (as) pia umesisitizwa umuhimu wa kutafuta elimu. Mtume (saw) anasema: “Kujifunza elimu ni faradhi kwa kila Muislamu.” Hatua ya kusisitizwa sana elimu na kufikia daraja ya ulazima wa kidini, inaonyesha ni kiasi gani Uislamu unavyotilia umuhimu suala zima la elimu na kupambana na ujinga. Mbali na hayo Mtume anasema: “Tambueni kuwa, Mwenyezi Mungu anampenda mtu anayetafuta elimu yoyote ile.” Maneno haya ya Mtukufu Mtume (saw) yanaonyesha kuwa, elimu haina kiwango wala mpaka bali elimu haiwezi kuwa na mwisho. Kwa ajili hiyo ikiwa mtu atajifunza elimu kwa kiwango chochote, basi atakuwa katika radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini wale wanaofanya juhudi zaidi katika njia hiyo, kwa hakika watakuwa wenye kupendwa zaidi. Kuhusiana na suala hilo Sayyid Muhammad Hussein Twabatwabai msomi na mfasiri mkubwa wa Qur’ani Tukufu anatafsiri aya ya  9 ya Surat Zumarnayosema: “Je afanyaye ibada wakati wa usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa Akhera na kutarajia rehema za Mola wake…. (ni sawa na  asiyefanya hayo)? Sema: Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.” Allamah Twabatwabai anaamini kuwa, katika aya hiyo suala la kuwa na elimu na kutokuwa na elimu kwa pamoja limetajwa katika namna ya mutlaqi. Lakini madhumuni yake ni elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu, kwa kuwa elimu hiyo ndiyo inayomfikisha mwanadamu kwenye ukamilifu na ndio uhalisia wa neno manufaa. Aidha kutokuwa na elimu hiyo kunamsababishia mwanadamu madhara makubwa. Lakini elimu nyinginezo, ni kama mali na utajiri ambazo manufaa yake ni kwa ajili ya maisha ya humu duniani na ni zenye kuishia hapa hapa duniani. Hivyo hadi sasa tuna makundi mawili ya wasomi, msomi muuminina msomi asiye muumini. Kundi la kwanza ndilo linalopendekezwa zaidi na ndilo pia lililo bora. Kadhalika Mwenyezi Mungu anasema: “Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba Mwanadamu katika pande la damu. Soma na Mola wako ni Mtukufu mno. Ambaye amefunza (kuandika) kwa kalamu. Amemfunza mwananadamu asilolijua.” Surat Alaq aya ya 1-5. Katika aya hizi kumetajwa daraja na hadhi ya uepo wa mwanadamu. Daraja bora zaidi ya mwanadamu ni ile ya mtu aliyesoma na kuelimika.







WABILLAHI TAUFIQ

Sunday, 8 January 2017

UTEUZI WA VIONGOZI WAPYA WA JUMUIYA YA MSATEKU







ASSALAM ALAYKUM WARAHMATU LLAHI WABARAKATUH

Jumuiya ya wanafunzi  kiislamu wa Teofilo Kisanji ambayo ipo chini ya Tamsya Mkoa wa Mbeya, leo tarehe 08/01/2017 imepata viongozi wapya katika ngazi mbalimbali za jumuiya hiyo. Viongozi hao walitangazwa na Katibu mkuu wa Tamsya wa Mkoa wa Mbeya na baadae kuridhiwa na wanajumuiya wote ambao walihudhuria katika hafla hiyo. Miongoni mwa viongozi walioteuliwa walikuwa ni kama ifuatavyo:
Amir wa jumuiya: Adnan Imran
Amirat wa jumuiya: Tatu Amour



Viongozi wengine ni manaibu Amir na Amirat wa jumuiya, makatibu wa jumuiya, pia maamiri na makatibu wa idara mbalimbali za jumuiya ikiwemo idara ya uchumi, idara ya habari na mawasiliano, idara ya elimu, idara ya daa'wa na maadili pamoja na idara nyenginezo.

 


Tunamuomba Allah (sw) amfanyie wepesi Amir wetu mpya katika kuiongoza jumuiya hii pamoja na viongozi wengine wanaomsaidia ili kufikia malengo ya jumuiya pamoja na kuipeleka mbele dini yetu ya uislam.



                                                         WABILLAHI TAUFIQ